Dar es Salaam. ‘Kivumbi leo’ hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za mafuta
zitakazotumika Septemba ambazo zimepaa huku maumivu zaidi yakiwa katika bei ya
dizeli.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa
jana Jumanne Septemba 5, 2023 saa 4 usiku na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo,
Dk James Mwainyakule imeonesha kuwa kuanzia leo Jumatano Septemba 6 jijini Dar
es Salaam petroli itauzwa Sh3,213 na dizeli itauzwa kwa Sh3,259.
Bei hizo zinamaanisha kuwa katika
Mkoa wa Dar es Salaam petroli imeongezeka kwa Sh14 kutoka Sh3,199 ya Agosti
huku dizeli ikiongezeka zaidi kwa Sh324.
Hata hivyo kwa upande wa mikoa
mingine yenye bandari zinazoshusha mafuta nchini pia bei ya mafuta imepaa;
Mtwara kwa mwezi huu lita moja ya petroli itauzwa Sh3,285 ikiongezeka kutoka
Sh3,271 na upande wa dizeli itauzwa Sh3,332 kutoka Sh3,008 mwezi uliopita.
Aidha, bei ya mafuta pia imepaa kwa
Mkoa wa Tanga ambapo kwa sasa lita moja ya petroli itauzwa Sh3,259 kutoka
Sh3,245 Agosti huku dizeli nayo ikiongezeka zaidi kutoka Sh2,981 Agosti hadi
Sh3,305.
Wakati hali ikiwa hivo katika mikoa
mitatu yenye bandari, pia bei itang’ata zaidi mkoani Kagera katika eneo la
Kyerwa (Ruberwa) ambapo petroli itauzwa Sh3,450 kwa lita na dizeli itauzwa
Sh3,497.
Kuhusu sababu ya kupanda kwa mafuta,
Mkurugenzi wa Ewura amesema gharama za uagizaji katika soko la dunia na maamuzi
ya kisiasa wa nchi wazalishaji mafuta zimechochea.
“Mabadiliko ya bei za mafuta kwa
Septemba 2023 yanatokana na kupanda kwa gharama katika soko la dunia kwa hadi
asilimia 21, gharama za uagizaji wa mafuta hadi asilimia 62 ikilinganishwa na
Agosti,”
“Pia, maamuzi ya kisiasa katika nchi
zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC+) imekuwa chanzo,” ameongeza.
Hali kama hii ya kupanda kwa bei za
mafuta ilitokea mwaka jana ambapo Serikali Mei 2022 iliweka ruzuku ya Sh100
bilioni katika bidhaa hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi ili kupoza bei yake. Na
Januari 2023 iliiondoa ruzuku hiyo.
Kwa habari za haraka na zauhakika zaidi endelea kutembelea website ya https://dirampya.blogspot.com/ ili uwe wa kwanza kupata habari.
No comments